1Alif Lam Ra. (A.L.R.) Hichi ni Kitabu tulicho kiteremsha kwako ili uwatowe watu kwenye giza uwapeleke kwenye muwangaza, kwa idhini ya Mola wao Mlezi, uwafikishe kwenye Njia ya Mwenye nguvu, Msifiwa!
3Wale wanao fadhilisha maisha ya dunia kuliko Akhera, na wanawazuilia watu wasifuate Njia ya Mwenyezi Mungu, na wanataka kuipotosha. Hao wamepotelea mbali.
4Na hatukumtuma Mtume ila kwa ulimi wa kaumu yake ili apate kuwabainishia. Basi Mwenyezi Mungu humuacha akapotea amtakaye, na akamwongoa amtakaye. Naye ni Mtukufu Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
5Na tulimtuma Musa pamoja na miujiza yetu, tukamwambia: Watoe watu wako kwenye giza uwapeleke kwenye mwangaza. Na uwakumbushe siku za Mwenyezi Mungu. Hakika katika hayo zipo ishara kwa kila mwenye kusubiri akashukuru.
6Na Musa alipo waambia watu wake: Kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu aliyo kujaalieni, pale alipo kuokoeni kutokana na watu wa Firauni walio kupeni adhabu mbaya kabisa, wakiwachinja wenenu wanaume, na wakiwawacha hai wanawake. Na katika hayo ulikuwa mtihani mkubwa unao toka kwa Mola wenu Mlezi.
9Je! Hazikukufikieni khabari za walio kabla yenu? Kaumu ya Nuhu, na A'adi, na Thamud, na walio baada yao, ambao hapana awajuaye ila Mwenyezi Mungu? Mitume wao waliwajia kwa hoja zilizo wazi, na wao wakarudisha mikono yao kwenye vinywa vyao, wakasema: Hakika sisi tumeyakataa hayo mliyo tumwa, na hakika sisi tuna shaka kubwa na mnayo tuitia.
10Mitume wao wakasema: Ati pana shaka na Mwenyezi Mungu, Muumba mbingu na ardhi? Yeye anakuiteni apate kukufutieni madhambi yenu, na akupeni muhula mpaka muda ulio wekwa. Wakasema: Nyinyi si chochote ila ni wanaadamu kama sisi. Mnataka kutuzuilia na waliyo kuwa wakiabudu baba zetu. Basi tuleteeni hoja ilio wazi.
11Mitume wao wakawaambia: Sisi kweli si chochote ila ni wanaadamu kama nyinyi. Lakini Mwenyezi Mungu humfanyia hisani amtakaye katika waja wake. Wala sisi hatuwezi kuleta uthibitisho ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na juu ya Mwenyezi Mungu ndio wategemee Waumini.
12Na tuna nini hata tusimtegemee Mwenyezi Mungu, na hali Yeye ametuongoa kwenye Njia zetu. Na hapana shaka sisi tutayavumilia hayo maudhi mnayo tuudhi. Na juu ya Mwenyezi Mungu wategemee wanao tegemea.
13Na walio kufuru wakawaambia Mitume wao: Tutakutoeni katika nchi yetu, au mrudi katika mila yetu. Basi Mola wao Mlezi aliwaletea wahyi: Hakika tutawaangamiza walio dhulumu.
17Awe anayagugumia, wala hawezi kuyameza. Na mauti yawe yanamjia kutoka kila upande, naye wala hafi. Na zaidi ya hayo ipo adhabu nyengine kali vile vile.
18Mfano wa walio mkufuru Mola wao Mlezi - vitendo vyao ni kama jivu linalo peperushwa kwa nguvu za upepo katika siku ya mdharba. Hawawezi kupata chochote katika waliyo yafanya. Huko ndiko kupotelea mbali.
21Na wote watahudhuria mbele ya Mwenyezi Mungu. Wanyonge watawaambia walio takabari: Sisi tulikuwa wafwasi wenu; basi hebu hamtuondolei kidogo hivi katika adhabu ya Mwenyezi Mungu? Watasema: Lau Mwenyezi Mungu angeli tuongoa basi hapana shaka nasi tungeli kuongoeni. Ni mamoja kwetu tukipapatika au tukisubiri; hatuna pa kukimbilia.
22Na Shet'ani atasema itapo katwa hukumu: Hakika Mwenyezi Mungu alikuahidini ahadi ya kweli. Nami nalikuahidini; lakini sikukutimizieni. Na sikuwa na mamlaka juu yenu, isipo kuwa nilikuiteni, nanyi mkaniitikia. Basi msinilaumu mimi, bali jilaumuni wenyewe. Mimi siwezi kuwa mtetezi wenu, wala nyinyi hamwezi kuwa watetezi wangu. Hakika mimi nilikataa tangu zamani kunishirikisha na Mwenyezi Mungu. Hakika madhaalimu watakuwa na adhabu chungu.
23Na walio amini na wakatenda mema wataingizwa katika Mabustani yapitayo mito kati yake, wadumu humo kwa idhini ya Mola wao Mlezi. Maamkio yao humo yatakuwa: Salaam.
27Mwenyezi Mungu huwatia imara wenye kuamini kwa kauli ya imara katika maisha ya dunia na katika Akhera. Na Mwenyezi Mungu huwaacha kupotea hao wenye kudhulumu. Na Mwenyezi Mungu hufanya apendavyo.
31Waambie waja wangu walio amini, washike Swala, na watoe katika tulivyo waruzuku, kwa siri na dhaahiri, kabla haijafika Siku isiyo kuwa na biashara wala urafiki.
32Mwenyezi Mungu ndiye aliye ziumba mbingu na ardhi, na akateremsha maji kutoka mbinguni. Na kwa hayo akatoa matunda kuwa ni riziki yenu. Na akafanya yakutumikieni majahazi yanayo pita baharini kwa amri yake, na akaifanya mito ikutumikieni.
34Na akakupeni kila mlicho muomba. Na mkihisabu neema za Mwenyezi Mungu hamwezi kuzidhibiti. Hakika mwanaadamu ni dhaalimu mkubwa, mwenye kuzikufuru neema.
36Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika hayo yamewapoteza watu wengi. Basi aliye nifuata mimi huyo ni wangu, na aliye niasi, hakika Wewe ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
37Mola wetu Mlezi! Hakika mimi nimewaweka baadhi ya dhuriya zangu katika bonde lisilo kuwa na mimea, kwenye Nyumba yako Takatifu, ewe Mola wetu Mlezi, ili washike Swala. Basi zijaalie nyoyo za watu zielekee kwao, na waruzuku matunda, ili wapata kushukuru.
38Ewe Mola wetu Mlezi! Hakika Wewe unajua tunayo yaficha na tunayo yatangaza. Na hapana kitu kinacho fichikana kwa Mwenyezi Mungu katika ardhi wala katika mbingu.
44Na waonye watu siku itapo wajia adhabu, na walio dhulumu waseme: Ewe Mola wetu Mlezi! Tuakhirishe muda kidogo tuitikie wito wako na tuwafuate Mitume. Kwani nyinyi si mliapa zamani kwamba hamtaondokewa?